Kufuatia kuidhinishwa rasmi hapo jana na baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuwa Katibu Mkuu mteule wa Umoja huo, Antonio Guterres leo ametangaza ramsi timu ya mpito itakayomsaidia katika maandalizi ya kuchukua hatamu mnamo Januari Mosi 2017.
Taarifa kutoka ofisi ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema kuwa walioingia katika timu hiyo ni Bi Kyung-wha Kang kutoka Korea Kusini atakayekuwa mkuu wa jopo hilo la mpito.
Bi Kang ambaye aliwahi kuwa Naibu Kamishina wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa na Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya kimataifa katika wizara ya mambo ya nje na biashara ya Korea Kusini, hivi sasa ni Naibu Mratibu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura.
Melissa Fleming.(Picha:UM/Jean-Marc Ferré)
Atakayekuwa mshauri mwandamizi na msemaji wake ni Bi Melissa Fleming kutoka Marekani. Amewahi kufanya kazi na mashirika mbalimbali kwenye upande wa habari na mawasiliano ikiwemo shirika la masuala ya usalama na ushirikiano barani Ulaya, OSCE, akijikita katika masuala ya haki za binadamu, kuzuia migogoro na maridhiano .
Pia amewahi kufanya kazi na shirika la kimataifa la nguvu za atomiki, IAEA. Hivi sasa ni mkuu wa mawasiliano na msemaji wa Kamishina mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.
Michelle Gyles-McDonnough.(Picha:UNDP)
Timu hiyo ya watu watano inamjumuisha pia Bi Michelle Gyles-McDonnough kutoka Jamaica, ambaye jukumu lake jipya litakuwa mshauri mwandamizi. Bi Mc Donnough amekuwa mwanasheria wa kujitegemea, lakini pia amekuwa mshauri wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa ya Amerika. Kwa upande wa Umoja wa Mataifa amehudumu na shirika la mpango wa maendeleo UNDP kama mratibu mkazi huko Malaysia, Singapore na Brunei Darussalam. Hivi sasa ni naibu mtawala na naibu mkurugenzi mteule wa kanda ya Asia na Pasifiki.
Bendera ya Portugal.(Picha:UM/Loey Felipe)
Mshauri mwandamizi mwingine katika jopo hilo atakuwa Bwana João Madureira wa Ureno. Ana uzoefu mkubwa wa masuala ya kidiplomasia nchini Ureno . Na kwa sasa analitumikia taifa lake kama waziri mshauri kwenye ubalozi wa kudumu wa Ureno kwenye Umoja wa mataifa.
Radhouane Nouicer.(Picha:UM/Violaine Martin)
Na hatimaye Bwana Radhouane Nouicer kutoka Tunisia atakuwa pia mshauri mwandamizi . Amefanya kazi na shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR kwa zaidi ya miaka 18 huko mashinani ikiwa ni pamoja na kuwa mkurugenzi wa ofisi ya Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini ya shirika hilo.
Aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa serikali ya mpito ya Tunisia mwaka 2011. Kwa sasa ni mshauri wa kikanda kwa ajili ya mgogoro wa kibinadamu waYemen.
Timu hii ya mpito itafanya kazi kwa karibu na maafisa wa Umoja wa Mataifa, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na asasi za kiraia ili kuhakikisha kipindi cha mpito kinapita pasi mushikheli wakati Guterres ambaye atakuwa Katibu Mkuu wa Tisa akijiandaa kuanza rasmi majukumu yake.