Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango mpya wa UM kutokomeza Kipindupindu Haiti watangazwa

Mpango mpya wa UM kutokomeza Kipindupindu Haiti watangazwa

Umoja wa Mataifa umewasilisha mbele ya nchi wanachama mpango wake mpya wa kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu nchini Haiti.

Naibu Katibu Mkuu wa umoja huo Jan Eliasson amesema mpango huo una hatua mbili, ambapo ya kwanza ni kuimarisha jitihada za kutibu na kutokomeza Kipindupindu, ikijumuisha upatikanaji wa maji safi na salama na huduma za kujisafi.

Hatua ya pili ni kuandaa pendekezo juu ya usaidizi wa rasilimali kwa wananchi wa Haiti walioathirika na Kipindupindu baada ya mlipuko wa mwaka 2010, pendekezo ambalo litawasilishwa na Katibu Mkuu mbele ya wanachama kabla hajamaliza muda wake mwishoni mwa mwaka huu.

(Sauti ya Eliasson)

“Kauli ya jinsi ya kusaidia wananchi wa Haiti hivi sasa na baadaye ni mshikamano, kasi na suluhisho. Tunatarajia gharama ya mpango huu iwe dola Milioni 400 katika kipindi cha miaka miwili ijayo, ambapo kila hatua itagharimu dola Milioni 200.”

image
Athari za kimbunga Matthew nchini Haiti. (Picha:UN/Logan Abassi)
Akizungumza kwa njia ya video kutoka mji mkuu wa Haiti, Port au Prince, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Sandra Honore amesema bado Kipindupindu ni tishio nchini humo na kimbunga Matthew kimefanya hali kuwa mbaya zaidi..

(sauti ya Sandra)

 “Kwa mantiki hiyo, mpango mpya wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kukabili Kipindupindu nchini Haiti, unakaribishwa zaidi wakati huu kuliko hata hapo awali. Washiriki wenzangu wa mazungumzo kutoka serikalini pamoja na wanasiasa wanasubiri kwa hamu utekelezaji wa mpango huo na mipango yake ya usaidizi ya muda mfupi, kati na mrefu ya kutokomeza ugonjwa huo.”