Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ethiopia na Sudan Kusini rejesheni watoto waliotekwa Gambella:UM

Ethiopia na Sudan Kusini rejesheni watoto waliotekwa Gambella:UM

Miezi sita baada ya kutekwa watoto 159 kwenye jimbo la Gambella Ethiopia, watoto 68 bado hawajulikani waliko.

Sasa wataalamu wawili wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wameitaka serikali ya Ethiopia na Sudan Kusini kuanza mara moja juhudi za pamoja kuhakikisha watoto ambao bado hawajulikani waliko wanarejea nyumbani.

Tarehe 15 Aprili 2016, watu wenye silaha kutoka kundi la kabila la Murle waliripotiwa kushambulia vijiji 13 vya kabila la Nuer kwenye wilaya za Jikaw na Lare jimbo la Gambella Ethiopia.

Shambulio hilo lilikatili maisha ya watu 208 na utekaji wa watoto 159, huku watu wengine 80 wakijeruhiwa na ng’ombe zaidi ya 2000 kuibwa.

Wataalamu hao mwakilishi maalumu dhidi ya uuzaji wa watoto Maud de Boer-Buquicchio na wa kuhusu mauaji Agnes Callamard, wameonya kwamba watoto hao 68 ambao wote wana umri wa chini ya miaka 13 wako katika hatari kubwa ya kuuzwa au kutumiwa vibaya na watekaji wao.

Wamezitaka serikali za Ethiopia na Sudan Kusini kuchukua hatua kuhakikisha vitendo kama hivyo vya kikatili havitokeo tena.