Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nitatumia zaidi diplomasia kusaka kurejesha amani duniani- Guterres

Nitatumia zaidi diplomasia kusaka kurejesha amani duniani- Guterres

Katibu Mkuu mteule wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kipaumbele chake cha kwanza ni kushughulikia ukosefu wa amani duniani ambao amesema ndio changamoto kubwa hivi sasa.

Amesema hayo akihojiwa kwa mara ya kwanza kabisa na Radio ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani baada ya kupitishwa na Baraza Kuu.

Bwana Guterres amesema  mizozo ya zamani imeendelea kuwepo, mipya ikiibuka huku ukwepaji sharia ukizidi kushamiri hivyo amesema..

(Sauti ya Guterres)

“Ongezeko la matumizi ya diplomasia katika kusaka amani litakuwa kipaumbele changu. Nafahamu kuwa hiyo inategemea zaidi nchi wanachama kwani Katibu Mkuu ana ukomo. Lakini nikifanya  kazi kama mratibu, au mhamasishaji na siyo dalali,  nadhani itawezekana kujumuisha wanachama wengi zaidi ili waelewe kuwa katika dunia ya leo, vita tulivyo navyo vinatia kichefuchefu.”

Alipoulizwa kwenye utendaji wa wadhifa wa ukatibu mkuu, lipi ambalo linamtia jakamoyo..

(Sauti ya Guterres)

"Kuna changamoto kubwa kuhusiana na marekebisho ya chombo hiki kiweze kuwa na ufanisi na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa watu tunaowahudumia ulimwenguni kote.”

Suala la nafasi ya wanawake katika nafasi za juu kwenye Umoja wa Mataifa lilikuwa miongoni mwa maswali na Katibu Mkuu Mteule akasema.

(Sauti ya Guterres)

 “Nadhani ni jambo muhimu, Usawa una maana kwamba iwapo Katibu Mkuu ni mwanamke, Naibu wake awe mwanaume na kama Katibu Mkuu ni mwanaume basi Naibu wake awe mwanamke.”

Bofya hapa kupata mahojiano kamili kati ya Bwana Guterres na Madiha Sultani wa Radio ya Umoja wa Mataifa.