Skip to main content

Ni kazi ngumu kupunguza athari za silaha kwa watoto katika migogoro:Zerrougui

Ni kazi ngumu kupunguza athari za silaha kwa watoto katika migogoro:Zerrougui

Jumuiya ya kimataifa ina jukumu kubwa la kupunguza athari za utumiaji wa silaha kwa watoto katika migogoro. Hayo yamesemwa na Bi Leila Zerrougui, mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto katika migogoro ya silaha alipowasilisha ripoti yake ya kila mwaka kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hi leo.

Amesema vita hivi na migogoro vimesababisha vifo na kuwalemaza maelfu ya watoto huku vikilazimisha mamilioni kukimbia wakitafuta usalama kuanzia Sudan Kusini, Syria na Yemen na kuna haja ya kuchukuliwa kwa hatua katika ngazi zote.

Mjumbe huyo amesema matumizi ya shughuli za anga na silaha zakulipuka yameleta madhara makubwa katika maeneo yenye wakazi wengi ikiwemo taasisi za afya na wafanyi kazi wake kupata majeruhi mara kwa mara na ametoa wito wa kuepukana na utumiaji wa silaha hizi kwenye maeneo hayo.

Pia amepongeza juhudi za Colombia na kundi la FARC-EP kwa watoto kuondolewa kwenye mzozo ijapokuwa matokeo ya kura ya maoni ya mkataba wa amani hayakuwa mazuri. Bi Zerrougui ameelezea wasi wasi wake juu ya watoto wanowekwa vizuizini kwa kuhusishwa na makundi ya waasi na kupitia juhudi za Umoja wa Mataifa wavulana karibu 50 nchini Sudan na Somalia wameachiliwa huru hivi karibuni.

Mjumbe huyo amesifu kuundwa kwa ajenda mpya ya maendeleo endelevu ya kuleta mabadiliko kwa watoto walioathirika na vita akitoa rufaa yake kwa juhudi za kuleta amani na kuzuia na kutafuta suluhisho ya migogoro pamoja na kupunguza idadi ya ukiukaji dhidi ya watoto.