Skip to main content

Mmeniteua kwa kauli moja na nitawahudumia kwa usawa- Guterres

Mmeniteua kwa kauli moja na nitawahudumia kwa usawa- Guterres

Niliposikia uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kunipendekeza kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hisia zangu zingaliweza kuelezewa kwa maneno mawili; Shukrani na unyenyekevu. Ndivyo alivyoanza hotuba yake Antonio Guterres baada ya Baraza Kuu kuridhia uteuzi wake wa kushika wadhifa huo kwa miaka mitano kuanzia Januari mwakani.

Guterres akatoa shukrani kwa nchi wanachama kwa heshima waliyompatia na imani yao kwake akisema..

(Sauti ya Guterres)

“Kwa kuchaguliwa na nchi wanachama, lazima niwahudumie wote kwa usawa na bila ajenda yoyote zaidi ya ile moja tu iliyomo kwenye Katiba ya Umoja wa Mataifa.”

Akaangazia majanga duniani akisema kwa miaka 10 amesafiri na kushuhudia machungu ya watu na akajiuliza.

(Sauti ya Guterres)

“Jambo gani limetukinga dhidi ya kushughulikia wanaokumbwa na shida za kiuchumi na kijamii. Yote haya yananifanya nihisi wajibu mkubwa wa kuweka mbele utu wa binadamu kwenye kazi yangu, na naamini jukumu kuu letu sote.”

Awali wawakilishi wa kanda mbali mbali walipata fursa ya kutoa neno ambapo ukanda wa Afrika uliwakilishwa na Balozi Abdallah Wafy wa Niger ambaye pamoja na kumpongeza Guterres amesema..

image
Balozi Abdallah Wafy wa Niger.(Picha:UM/Cia Pak)
(Sauti ya Balozi Wafy)

“Kundi la Afrika linasubiri kwa hamu mkutano ujao usio rasmi na Katibu Mkuu mteule tarehe 19 mwezi Oktoba ambapo ni fursa ya kipekee ya kushiriki kwenye masuala ya kipaumbele na muhimu wa kundi la AFrika, na zaidi ya yote jinsi ya kufanya Umoja wa Mataifa ukidhi mahitaji ya uwepo wake.”

Kuwait iliwakilisha ukanda wa Asia na Pasifiki na Balozi Mansour Al Otabi akasema..

image
Balozi Mansour Al Otabi wa Kuwait.(Picha:UM/Amanda Voisard)
(sauti ya Balozi Otabi)

Nchi wanachama wa kundi la Asia na Pasifiki linaahidi ushirikiano wake thabiti kwa Guterres anapokabiilana na changamoto mpya na zinazoibuka.”

Kutoka Ukanda wa Ulaya Mashariki, Balozi Kaha Imnadze wa Georgia, pamoja na pongezi akasema wanaunga mkono stadi zilizoonyeshwa na wagombea wote ikiwemo wale waliotoka ukanda wa Ulaya Mashariki na kwamba..

(Sauti ya Balozi Kaha)

image
Balozi Kaha Imnadze wa Georgia.(Picha:UM/Cia Pak)
“Tunasalia na harakati za kubaini mbinu mpya za kuendelea kuimarisha mchakato wa uteuzi, ikiwemo kuendeleza uwiano wa kijinsia na kikanda wakati wa uchaguzi wa maafisa wa nafasi za juu katika Umoja wa Mataifa.”

Balozi Matthew Rycroft wa Uingereza akazungumza kwa niaba ya ukanda wa Ulaya Magharibi akimpongeza Guterres na kwamba uteuzi wake umekuja wakati wa changamoto nyingi. Amesema Umoja wa Mataifa thabiti unatakiwa zaidi hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote kwa hiyo..

(Sauti ya Balozi Matthew)

image
Balozi Matthew Rycroft wa Uingereza.(Picha:UM/Cia Pak)
“Sasa ni juu yetu sisi, nchi wanachama kumuunga mkono Guterres, kushirikiana naye kwa karibu kwenye maamuzi yanayoweza kuendeleza, kuimarisha na kuufanya thabiti Umoja wa Mataifa unaposhughulikia changamoto kubwa duniani.”

Chile iliwakilisha ukanda wa Amerika Kusini na Karibea ambapo Balozi Cristian Barros Melet

(Sauti ya Balozi Melet)

image
Balozi Cristian Barros Melet wa Chile.(Picha:UM/Cia Pak)
“Tuna imani kuwa Bwana Guterres ataanzisha ari mpya ya kuendeleza amani na usalama duniani.”

Marekani ambayo ni nchi mwenyeji wa Umoja wa Matiafa ilipatiwa fursa na Balozi wake kwenye Umoja wa Mataifa Samantha Power akagusia suala la mvutano ndani ya Baraza la Usalama, mvutano ambao hukwamisha baadhi ya maazimio ya Umoja huo akisema..

image
Balozi Samantha Power wa Marekani.(Picha:UM/Cia Pak)
(Sauti ya Samantha)

"Kuchaguliwa kwa Antonio Guterres kuwa Katibu Mkuu wa 9 wa Umoja wa Mataifa, ni matokeo ya aina yake yanayokwenda sambamba na ongezeko la mahitaji ya ulimwengu ya kuwa na Umoja wa Mataifa ulio na nguvu zaidi. Na ni ajabu zaidi kwani-na hebu tuseme ukweli- mara nyingi hapa ndani ya Umoja wa Mataifa, ajenda finyu zinatutenganisha na kutuzuia kuchukua hatua zenye kuleta maendeleo. Uteuzi huu umezidi matarajio ya wengi, na lazima tuuelekeze kwenye masuala mengine. Wengi walidhani tutashindwa kuafikiana kuhusu uteuzi wa Katibu Mkuu na mmoja wao ni mimi."

Hivyo akasema..

(Sauti ya Samantha)

"Ili Umoja wa Mataifa ufanikiwe tunakuomba Bwana Guterres uwe msaka amani ili kusitisha vita vya kikatili Syria, Yemen na Sudan Kusini. Tunakuomba uwe mleta mabadiliko, urahisishe urasimu na uondoe mambo yasiyohitajika.Na tunakuomba uwe mtetezi, uhamasishe ulimwengu kuitikia majanga ya kibinadamu na majanga yanayosababishwa na binadamu, na kulinda haki ya raia wote bila kujali imani,utaifa,rangi au jinsia" 

image
Katibu Mkuu mteuele Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuteuliwa. (Picha:UN/Kim Haughton)
Baada ya kuidhinishwa kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, katibu mkuu mteule Antonio Guterres alikutana na waandishi wa habari ambapo aliulizwa kuhusu Syria..

(Sauti ya Guterres) 

"Mimi nina mshikamano na watu wa Syria. Nilipokuwa kamishna wa wakimbizi nilishudia ukarimu wa watu wa Syria wa kukaribisha wakimbizi kutoka Iraq na Palestina na kuwapa haki zao. Na kuona mateso wanayoyapata inanivunja moyo, nitafanya kadri ya uwezo wangu kujaribu kuleta amani ambayo ni maadili yetu na bila shaka katika nchi nyingine zilizo na mizozo Sudan Kusini, Yemen na kwingineko kwa uaminifu."