Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakunga wa jadi wathaminiwe:WHO

Wakunga wa jadi wathaminiwe:WHO

Shirika la afya ulimwenguni WHO na wadau limetaka kukomeshwa kwa unyanyasaji, ubaguzi na kutoheshimiwa kwa uwezo walionao wakunga wa jadi katika kutoa huduma kwa wanawake na watoto wachanga.

Shirika hilo la afya ulimwenguni linasema katika utafiti wake wa kwaza wa kimataifa kuhusu wakunga wa jadi, ulioratibiwa kwa pamoja na shirikisho la wakunga wa jadi ICM, na taasisi ya kifimbo chekundu WRA, ambao umepewa jina Sauti za wakunga wa jadi, Uhalisia wao, imebainika kwamba juhudi zao hukwamishwa na ukosefu wa usawa wa mamlaka katika mfumo wa afya huku pia wakitengwa na tamaduni,wakikosa malazi na mishahara kidogo.

Likinukuu kauli ya Mkurugenzi wa afya uzazi , watoto na vigori Dk Anthony Costello, WHO imesema ni wakati wa kutambua jukumu muhimu la wakunga wa jadi katika kutunza uhai wa akina mama na watoto wachanga. Dk Costello amesema kwa muda mrefu wakunga wa jadi wamepuuzwa ushirikishwaji katika meza ya uamuzi.

WHO imeeleza umuhimu wa kuwapatia usaidizi wa kitaalamu ikiwamo mazingira bora ya kazi, elimu thabiti,kanuni na uwakili kwa kundi hilo la kiafya.

Kila mwaka zaidi ya wanawake 300 000 hufariki wanapojifungua na watoto wachanga takribani milioni tatu hufariki katika siku 28 za mwanzo za uhai wao kutokana na sababu ambazo zaweza kuzuilika.