Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaonya juhudi ziongezwe kukabili kifua kikuu

WHO yaonya juhudi ziongezwe kukabili kifua kikuu

Shirika la afya ulimwenguni WHO, limeonya kuwa juhudi za kinga, utambuzi na tiba dhidi ya kifua kikuu zinahitaji kasi zaidi ili kufikia lengo namba tatu la afya bora la malengo ya maendeleo endelevu SDGs.

Katika ripoti yake kuhusu kifua kikuu TB, kwa mwaka 2016, WHO imesema serikali zilikubali kumaliza ugonjwa huo kupitia mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa, kwa kupunguza asilimia 90 ya vifo,asilimia 80 ya visa ifikapo 2030 ikilinganishwa na mwaka 2015.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Margaret Chan amenukuliwa katika ripoti hiyo akisema juhudi za ziada zinahitajika vinginevyo nchi zitaendelea kubaki nyuma katika makabiliano dhihi ya gonjwa hilo angamizi.

Juhudi za kutokomeza TB ziliokoa maisha ya watu milioni tatu mwaka 2015, lakini ripoti inasema kwamba utafiti unaonyesha kuwa kwa sasa hali ni mbaya kuliko makisioa ya awali na hii ni kwa mujibu wa utafiti nchini India.