Skip to main content

Hali ya Afar, Ethiopia ni mbaya kutokana na ukame- FAO

Hali ya Afar, Ethiopia ni mbaya kutokana na ukame- FAO

Viongozi wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO wametembelea eneo la Afar nchini Ethiopia, lililoshuhudia kiwango kikubwa cha madhara ya ukame uliosababishwa na El Nino kuanzia mwaka jana.

Wakati wa ziara hiyo Dominique Burgeon ambaye ni Mkurugenzi wa masuala ya dharura wa FAO pamoja na mwakilishi wa FAO nchini Ethiopia Amadou Allhoury walikutana na wafugaji ambao walipoteza mifugo yao kutokana na ukame.

Mmoja wa wafugaji hao alieleza jinsi ukame eneo hilo ulivyosababisha mifugo kufa kwa njaa kwa kutokana na uhaba wa malisho.

Mfugaji mwngine Mutha Ahmed alieleza kuwa licha ya kupoteza kondoo 50 na mbuzi bado hawezi kupata msaada kwa kuwa kipaumbele ni kwa familia zenye watoto wachanga na wenye ndama.

Bwana Burgeon baada ya ziara hiyo amesema hali ni mbaya kwenye eneo hilo na kwingineko ambako wanategemea mifugo.

Amesema ijapokuwa misaada imeelekezwa bado hawawezi kupuuza mahitaji ya lazima ili kustahimili athari za ukame.

Amesema FAO itashirikiana na mamlaka husika ili kuongeza juhudi hizo ambapo wameomba dola million 14 zaidi kwa ajili ya miradi mbali mbali katika sekta ya mifugo na mazao hadi mwisho wa mwaka 2016.