Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nigeria kinara wa kupunguza majanga : UM

Nigeria kinara wa kupunguza majanga : UM

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kupunguza athari za majanga, yenye kauli mbiu Ishi Usimulie, Umoja wa Mataifa umesema tangu kuaridhiwa kwa mkataba wa Sendai wa kupunguza majanga mwaka uliopita, Nigeria ni kielelezo cha utekelezaji wa mkataba huo kwa jinsi ilivyokabiliana na homa kali ya Ebola.

Kwa mujibu wa ujumbe wa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu kupunguza majanga Robert Glasser, mafaniko ya taifa hilo la Nigeria katika kudhibiti Ebola kwa kudhibiti idadi ya visa ambavyo haikuvuka 20 wakati gonjwa hilo hatari lilipoikumba Afrika Magharibi, ni mfano wa kuigwa.

Amesema mkataba wa Sendai unatambua afya kama janga la kukabiliana nalo na akaongeza kuwa taasisi ya SEEDS inatambuliwa kwa kupunguza hatari ya kimbunga kwenye jamii masikini India, serikali ya Fiji nayo ikitambuliwa kwa kujihadhari na kimbunga pamoja na Peru iliyojihami dhidi ya El Niño.

Mwakilishi huyo maalum wa Katibu Mkuu amesisistiza

(SAUTI GLASSER)

‘Kimbunga na Tsunami vinaongoza kwa ujumla katika kuuwa , ukiangalia majanga yatokanayo na hali ya hewa, kwanza yamengzeka zaidi ya mara mbili kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita, pili katika miaka 15 iliyopita, majanga yatokanayo na hali ya hewa yamekuwa chanzo kikuu cha vifo.’’

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ban Ki-moon katika ujumbe wake kuhusu siku hiyo,amezitaka nchi hususani zeanye kipato kidogo kuwekeza katika kuzuia majanga na kuondokana na utamaduni wa kuchukua hatua baada ya majanga.