Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP kutoa msaada wa chakula kwa waathirika wa kimbunga Matthew Cuba

WFP kutoa msaada wa chakula kwa waathirika wa kimbunga Matthew Cuba

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) likishirikiana na Serikali ya Cuba limo mbioni kupeleka chakula kwa watu 180,000 kusini mwa nchi hiyo, ambao wameaathirika zaidi na kimbunga Matthew.

Kwa mujibu wa shirika hilo, operesheni itaanza na utoaji wa mchele na maharage kwa wakazi wa mkoa wa Guantanamo hususan maeneo ya Baracoa, Maisi, Imías na San Antonio del Sur, ambayo ndio maeneo yaliyoathirika zaidi nchini Cuba.

WFP imesema, awamu ya kwanza ya operesheni hiyo itatumia akiba ya chakula iliyowekwa hapo kabla kwa ajili ya majanga, na itakwenda kwanza kwa watu wanaouhitaji zaidi. pia imetoa ombi la dola milioni 4 kwa wadau wa kimataifa kwa ajili ya kusaidia watu 180,000 katika miezi sita ijayo.

Pia shirika hilo limesema tathmini ya hali halisi bado inaendelea Cuba, na miongoni mwa baadhi ya athari za kwanza zilizodhahiri ni uharibifu wa chakula, sekta ya kilimo, nyumba na miundombinu.

Kimbunga Matthew kimeweka rekodi ya kimbunga chenye dhoruba kali zaidi kuwahi kutokea mashariki mwa Cuba katika miaka tisa iliyopita.