Mikutano na makongamano haishibishi watu- Nwanze
Rais wa shirika la kimataifa la ufadhili wa maendeleo ya kilimo, IFAD , Kanayo Nwanze amesema ahadi za viongozi wa Afrika za kuleta mapinduzi ya kilimo zitatimia iwapo wao wenyewe kwanza watashawishika kuwa sekta hiyo ni msingi wa kuondoa umaskini kuliko sekta yoyote ile.
Bwana Nwanze amesema hayo alipohojiwa na Joshua Mmali wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa akieleza kuwa maneno pekee hayatoshi kama hakuna vitendo...
(Sauti ya Nwanze-1)
“Nadhani tatizo ni kwamba kwanza kabisa tunahitaji kuangalia iwapo tuna viongozi wenye dira walioazimia na wanaoelewa kuwa huwezi kuzungumzia maendeleo ya taifa iwapo utapuuza takwimu. Na pia wanapaswa kuwa na taasisi, taasisi zinazoweza kutekeleza, halikadhalika utawala wa kisheria.”

(sauti ya Nwanze-2)
“Nadhani watu wanapaswa kuzungumza, na kudai vitendo, vitendo vizidi maneno ya mikutano, makongamano na maazimio. Mikutano hailishi watu. Ahadi hazishibishi watu.Kile kinacholisha watu ni vitendo vinavyofanyika mashinani na tunapaswa kuweka pesa pale inapohitajika.”