Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yatoa wito wa kutoza kodi ya vinywaji vyenye sukari

WHO yatoa wito wa kutoza kodi ya vinywaji vyenye sukari

Kutoza kodi na kupandisha juu bei ya vinywaji vitamu ndio suluhu pekee katika kuboresha maisha ya mamilioni ya watu ulimwenguni kote, imesema Shirika la Afya Duniani(WHO) leo, wakati wa maadhimisho ya siku ya kukabiliana na utipwatipwa duniani.

Mapendekezo hayo yanatokana na utafiti wa kina uliofanywa na shirika hilo, ambalo limeonyesha jinsi kupanda kwa bei ya vinywaji vyenye sukari nyingi kunavyoweza kwenda sambamba na kushuka kwa matumizi yake. WHO inasema kuwa zaidi ya nusu bilioni ya watu duniani kote ni tipwatipwa huku zaidi ya milioni 400 wanaugonjwa wa kisukari na idadi hii inaongezeka kwa kasi.

Dkt. Francesco Branca, Mkurugenzi wa kitengo cha Lishe, Afya na Maendeleo, WHO, anasema wakati huu ni wakati wa kuchukua hatua zaidi ikiwa ni pamoja na kushirikisha serikali katika kubadili sera kwani..

(Sauti ya Francesco)

"Tumejadili suala la sukari mwaka uliopita, na WHO imetoa pendekezo la kushusha sukari, lakini badala yake utumiaji sukari umepanda zaidi katika maeneo mengine duniani, na hilo linaleta wasiwasi mkubwa. Na muhimu katika sukari, ni vinywaji vyenye sukari kwani ni rahisi sana kuingiza kiwango kikubwa cha sukani mwilini na hupatikana kiurahisi katika maeneo mengi duniani".

WHO imesema ingawa Marekani ndio iliyoshika usukani kimataifa katika matumizi makubwa ya vinywaji vyenye sukari, tatizo hilo sasa pia limeenea Amerika ya Kusini, China na Kusini mwa Jangwa la Sahara.