WHO yahofia mlipuko zaidi wa kipindupindu baada ya kimbunga Haiti
Hofu ya shirika la afya ulimwenguni WHO kuhusu hatari ya visa zaidi vya kipindupindu Haiti baada ya kimbunga Matthew imeongezeka. Shirika hilo linasema katika eneo la Grand’Anse visa vimeongezeka na kufikia 148, Sud 53 , huku visa vipya 28 vikiripotiwa mjini Artibonite
WHO na shirika la afya kwa mataiifa ya Amerika PAHO wanaongeza jitihada za kukabiliana na mlipuko huo na wanaishauri serikali ya Haiti kutekeleza mipango ya kitaifa ya kudhibiti kipindupindu huku wakizingatia athari za kimbunga. Dr Dominique Legros ni mratibu wa masuala ya kipindupindu katika WHO
(SAUTI YA DR DOMINIQUE)
“La msingi ni kwamba tumeshuhudia kupungua kwa visa kati ya mwanzo wa mlipuko 2010 na 2013-2014, idadi ilikuwa ndogo sana, lakini tangu 2014 kila mwaka tunashuhudia tena ongezeko la visa na mwaka 2016 tumeona visa vingi zaidi ya 2015, sababu ni rahisi, watu bado hawana fursa ya maji safi."
Zaidi ya wahudumu wa afya 80 kutoka WHO na PAHO wamepelekwa Haiti kukabiliana na athari za kimbunga Matthew