Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto wa kike ni kitovu cha kufanikisha SDGs- Ban

Mtoto wa kike ni kitovu cha kufanikisha SDGs- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ustawi, haki za binadamu na uwezeshaji wa watoto wa kike Bilioni Moja nukta Moja ulimwenguni kote ni kitovu cha mafanikio ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Ban amesema hayo katika ujumbe wake wa siku ya mtoto wa kike hii leo, maudhui yakiwa ni maendeleo ya mtoto wa kike ni maendeleo ya SDGs, kipi muhimu kwa mtoto wa kike.

Amesema Umoja wa mataifa umeazimia kumaliza ubaguzi na ghasia dhidi ya mtoto wa kike, sambamba na mila potofu kama vile ndoa katika umri mdogo.

Kwa mantiki hiyo amesema ahadi imeshatolewa hakuna mtu atakayeachwa nyuma kwenye malengo hayo,  wakati huu ambapo mara nyingi vijijini na hata kwenye kambi za wakimbizi watoto wa kike husahaulika.

Amesema kuwekeza kwa mtoto wa kike ni jambo la msingi kufanya na bora vile vile, hivyo ametaka kila mtu kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha watoto wote wa kike wanajumuishwa kwani kila mtoto wa kike ana umuhimu.