Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awapongeza viongozi wa Colombia

Ban awapongeza viongozi wa Colombia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, leo amempongeza Rais wa Colombia, Juan Manuel Santos kwa ushindi wake wa tuzo ya amani ya Nobel.

Akizungumza kwa njia ya simu, Ban pia amempogeza Kamanda Timoleon Jiménez kwa juhudi zake za kuleta amani na amewasihi viongozi hao wawili kuendeleza moyo wa kupigania amani licha ya matokeo ya kura ya maoni ya hivi karibuni, yaliyopinga mkataba wa amani nchini Colombia.

Amesema kilicho muhimu zaidi katika ushindi huo wa tuzo ya amani ya Nobel, ni ujumbe unaokuja katika wakati muafaka kwa wahanga wa migogoro, ambao walikuwa katikati ya mazungumzo ya amani ya Havana.

Ban amekaribisha dhamira ya vyama pinzani ya kuendelea na usitishaji wa mapigano, na vile vile ahadi ya kupitishwa kwa itifaki ya kuzuia matukio yoyote, na jukumu lililopewa la mchakato wa ufuatiliaji wa pande tatu (MVM) wa kuhakikisha utekelezwaji wa itifaki hiyo.

Kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu Ban amesema anaamini kwamba hatua hizi zitasaidia kujenga mazingira mazuri kwa ajili ya majadiliano ya kisiasa ambayo anatumai yatahitimisha kwa mafanikio mchakato wa amani.