Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ombi la dola Milioni 120 kusaidia Haiti lazinduliwa leo

Ombi la dola Milioni 120 kusaidia Haiti lazinduliwa leo

Jitihada kubwa zinatakiwa ili kukwamua Haiti kufuatia athari za kimbunga Matthew, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alipozungumza na wanahabari hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Ban amesema kando ya vifo, watu milioni 1.4 wanahitaji misaada, shule 300 zimeharibiwa na baadhi ya miji na vijiji vimesambaratishwa.

Amesema fedha za awali zimetolewa, tathmini ya madhara ya kimbunga inaendelea kufanyika lakini bado msaada zaidi unahitajika hivyo..

(Sauti ya Ban)

“Leo huko Geneva, tumezindua ombi la dharura la dola Milioni 120 kukidhi mahitaji ya kibinadamu yanayotolewa na Umoja wa Mataifa kwa miezi mitatu ijayo. Athari za kimbunga ni pamoja na ongezeko la hatari ya magonjwa yanayoenezwa kwa maji ikiwemo kipindupindu.”

Katibu Mkuu akazungumzia pia mashambulizi dhidi ya maeneo ya raia huko Yemen, mashambulizi ambayo hadi sasa wahusika wanakwepa mkono wa sheria.

(Sauti ya Ban)

“Janga linalotengenezwa na binadamu linaendelea kuchipuka mbele ya macho yetu. Ukwepaji mkono wa sheria imezidisha machungu. Licha ya ongezeko la uhalifu unaofanywa na pande zote kwenye mzozo, bado hatujaona matokeo ya uchunguzi wowote halali.”

Katibu Mkuu amerejelea wito kwa Kamishana Mkuu wa Haki za binadamu wa kutaka Baraza la haki za binadamu liunde chombo  huru na cha kimataifa kitakachochunguza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Yemen.

Ban akaulizwa kuhusu Baraza la Usalama kushindwa kuafikiana kuhusu mustakhbali wa Syria licha ya Katibu Mkuu kuelezea kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

(Sauti ya Ban)

 “Hali huko Aleppo kwa kweli inavunja moyo. Nilisikitika sana siku ya Jumamosi ambapo Baraza la Usalama lilishindwa tena kuungana. Hakuna muda kama huo wa kujadili na kupingana juu ya jambo ambalo Baraza la Usalama linapaswa kuamua. Jibu ni wazi kuwa wanapawa kufanya kazi pamoja kulinda maisha ya watu na kupatia suala hili suluhu la kisiasa.