Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi ya aibu Yemen hayapaswi kuendelea- Zeid

Mashambulizi ya aibu Yemen hayapaswi kuendelea- Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amesisitiza wito wake wa dharura wa kufanyika kwa uchunguzi wa kimataifa nchini Yemen kufuatia shambulio la mwishoni mwa wiki dhidi ya waombolezaji, shambulio alilolielezea kuwa ni la aibu.

Katika taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya haki za binadamu, Kamishna Zeid amesema tangu kuanza kwa mzozo Yemen, harusi, maeneo ya masoko, hospitali na shule na hivi karibuni mazishi yamekuwa yakilengwa na kusababisha idadi kubwa ya vifo vya raia huku wahusika hawachukuliwi hatua yoyote.

Amesema shambulio la juzi lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 140 limefanyika wiki chache baada ya Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kutupilia mbali wito wake wa kutaka uamuzi wa kuundwa kwa chombo huru cha kimataifa kuchunguza kwa kina ukiukwaji wa sheria za kimataifa ikiwemo uhalifu wa kivita nchini Yemen.

Kamishna Zeid amesema kitendo cha baraza kushindwa kuunda chombo cha kimataifa kinaweka mazingira ya ukwepaji sheria na hivyo amesema mashambulizi hayo ya aibu hayapaswi kuendelea.