Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulizi la anga Yemen laua zaidi ya watu 140, Ban alaani vikali

Shambulizi la anga Yemen laua zaidi ya watu 140, Ban alaani vikali

Waombolezaji zaidi ya 140 wameuawa kwa shambulio kutoka angani kwenye mji mkuu wa Yemen.

Shambulio hilo lilitokea wakati watu hao wakiwa kwenye ibada ya mazishi ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikal huku akitua salamu za rambirambi kwa wafiwa na majeruhi.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imemnukuu pia Ban akitaka uchunguzi wa haraka wa mashambulizi hayo kutoka angani yanayodaiwa kuwa yamefanywa na washirika wanaoungwa mkono na Saudia.

Ban amesema mashambulizi yoyote yale dhidi ya raia hayakubaliki na ametoa wito kwa wahusika kufikishwa mbele ya sheria.

Wakati huo huo, mratibu wa masuala ya kibindamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Jamie McGoldrick amesema wameshtushwa sana na shambulio hilo ambalo lilipiga jamii iliyokuwa kwenye maombolezo.

Ametaka ghasia dhidi ya raia nchini Yemen ikome mara moja na kutaka jamii ya kimataifa ishinikize pande kwenye mzozo husika zilinde raia.