Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Syria njia panda, Urusi yatumia kura turufu

Syria njia panda, Urusi yatumia kura turufu

Azimio lililowasilishwa na Ufaransa na Hispania mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili pamoja na mambo mengine lisitishe mashambulizi ya anga huko Aleppo nchini Syria, limegonga mwamba baada ya Urusi kutumia kura yake turufu kulipinga.

Azimio hilo liliwasilishwa hii leo katika kikao cha baraza hilo jijini New York, Marekani, ambapo licha ya kupata kura 11 kati ya 15,  halikuweza kupitishwa kwa kuwa Urusi ilipinga kwa kutumia kura yake turufu, Venezuela nayo ikilikataa huku nchi mbili ikiwemo Angola hazikuonyesha msimamo wowote.

Chimbuko la azimio hilo ni mwendelezo wa mashambulio ya anga huko Aleppo ambayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema yamegeuza mji huo kuzidi hata eneo la machinjio.

Pamoja na kutaka kusitishwa kwa mashambulio ya angani, azimio lililenga pia kutaka pande husika kushirikiana na bodi ya uchunguzi iliyoundwa na Katibu Mkuu kuchunguza shambulio la tarehe 19 Septemba dhidi ya msafara wa shirika la hilal nyekundu la Syria.

Akizungumza na wanahabari baada ya azimio hilo kutopishwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault amesema ni hatua ya kusikitisha kwani ililenga kuboresha maisha ya wananchi wa Syria ambao kutwa kucha wanakumbwa na mashambulizi.

Urusi nayo iliwasilisha azimio lingine kuhusu Syria ambalo kwa kiasi kikubwa lilifanana na lile la Ufaransa na Hispania, bila ya kipengele cha bodi ya uchunguzi, azimio ambalo nalo pia limegonga mwamba na kuacha mustakhbali wa Syria kwenye njia panda.