Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CERF yapigia chepuo harakati za usaidizi Haiti

CERF yapigia chepuo harakati za usaidizi Haiti

Mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF umetoa dola Milioni Tano kusaidia mahitaji muhimu kwa watu walioathiriwa na kimbunga Matthew.

Taarifa ya CERF imesema fedha hizo ni nyongeza ya mkopo wa dola Milioni Nane ambazo CERF ilipatia shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu nchini Haiti.

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya misada ya dharura, OCHA Stephen O’Brien amesema kimbunga hicho kimeleta madhara makubwa ikiwemo vifo vya mamia ya watu na maelfu ya familia wamepoteza makazi, mifugo na mazao.

Amesema kimbunga hicho kimerejesha nyuma harakati za Haiti za kujijenga upya baada ya tetemeko la ardhi na mlipuko wa Kipindupindu.

Kwa sasa mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wa kibinadamu wanashirikiana na serikali ya Haiti kutathmini kiwango kamili cha uharibifu na kutoa misaada zaidi.