Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Kigali ufanikishe mabadiliko ya itifaki ya Montreal- Ban

Mkutano wa Kigali ufanikishe mabadiliko ya itifaki ya Montreal- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo amepatiwa tuzo za uendelevu wa tabianchi kutokana na harakati zake za kuchagiza mikakati ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Amekabidhiwa tuzo hiyo huko Reykjavic, Iceland wakati wa mkutano wa kila mwaka wa jumuiko la Arctic, ncha ya kaskazini mwa dunia ambapo katika hotuba yake amesema tuzo hiyo kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya kiraia na wadau wote waliosimama kidete kutetea tabianchi.

Ban ametumia hotuba hiyo kuzungumzia mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi akisema hadi leo nchi 191 zimesharidhia na vigezo vyote viwili vimevukwa na mkataba utaanza rasmi mwezi ujao kama ilivyokwishatangazwa.

Katibu Mkuu akasema ni vema kutekeleza ahadi kwani mabadiliko ni dhahiri akitolea mfano eneo la ncha ya kaskazini akisema kiwango cha ongezeko la joto ni kikubwa kuliko kwingineko duniani hivyo maneno sasa yawe matendo.

image
Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-moon (kushoto) pamoja na ujumbe wake katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iceland Lilja Alfreðsdóttir na ujumbe wake(upande wa kulia) wakati wa mazungumzo. (Picha:UN/Rick Bajornas)
Amesema fedha zinahitajika hasa kwa nchi zinazoendelea ili ziweze kupunguza kiwango cha utoaji wa hewa chafuzi na kuhimili na kukabili madhara yasiyoepukika.

(Sauti ya Ban)

“Tunataka serikali zifikie maridhiano wiki ijayo huko Kigali kuhusu umuhimu wa kurekebisha itifaki ya Montreal, ambayo itaondoa hewa zinazochafua ukanda wa ozone, HFC. Hii inaweza kusaidia kupunguza kiwango cha joto kwa nusu nyuzijoto ifikapo mwishoni mwa karne hii.”

Baadaye katika mkutano na wanahabari uliohudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iceland Lilja Alfreðsdóttir, Ban amesisitiza umuhimu wa matumizi ya mitandao ya kijamii kuchagiza serikali, wanasiasa na wafanyabiashara kutekeleza mkataba wa Paris.