Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Manusura wa majanga wasaidiwe kisaikolojia kuwanusuru na magonjwa ya akili: Ban

Manusura wa majanga wasaidiwe kisaikolojia kuwanusuru na magonjwa ya akili: Ban

Ikiwa leo ni siku ya afya ya akili duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ni muhimu huduma za ugonjwa huo zipatikane kila mahali na kusisitiza katika kutoa huduma za kisaikolojia kwa manusura wa majanga.

Katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku hii ambayo mwaka huu inaangazia umuhimu wa usaidizi wa kisakolojia, Ban amesema dunia leo inashuhudia wimbi kubwa la dharura za kibinadamu zinazohusiana na machafuko na majanga ya asili na waathiriwa aghalabu hupata kama sio kukosa kabisa huduma za ushauri.

Amesema ni muhimu kuwafunza wanoshughulikia dharura kama vile maafisa wa polisi, maafisa wazima moto, na wahudumu wa misaada ya dharura namna ya kutoa misaada ya kisaikolojia kwa wahitaji.

Katika mahojiano na redio ya Umoja wa Mataifa mshauri wa afya ya akili kwa umma wa shirika la afya ulimwenguni WHO Dk. Mark Ommeren anasema jamii inahitaji kusaidia watu waliopatwa na viwewe kwa kushuhudia mambo ya kutisha na kuongeza.

( SAUTI DK MARK OMMEREN)

‘‘Moja ya vitu ambavyo watu waweza kufanya ni kuanza kuongea kuhusu ugonjwa wa akili, kuna unyanyapaa wa kiwango kikubwa kwa wagonjwa wa akili, pia kuhakikisha huduma za afya kwa wagonjwa hawa zinapatikana.’’

Kwa mujibu wa takwimu za WHO za mwaka jana, duniani kote kati ya watu 10 mmoja aliugua ugonjwa wa akili.