Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia wahitaji ulinzi Nigeria: UNHCR

Raia wahitaji ulinzi Nigeria: UNHCR

Raia Kaskazini mwa Nigeria bado wanakabiliwa na ukosefu wa usalama tangu mwanzoni mwaka huu kundi la kigaidi la Boko Haram liliposhika hatamu ya eneo hilo, watu hao wanakosa mahitaji muhimu, wanawake wakiwa hatarini zaidi limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Hayo ni metokea ya utafiti wa wafanyakazi wa UNHCR ambao wamekuwa wakiendesha uchunguzi kwa majuma mawili kuhusu mahitaji na hali katika jimbo la Borno.

Timu ya UNHCR na wadau wamewahoji viongozi wa kijamii na watu binafsi katika miji kadhaa ambapo pia wamebaini kuwa wakazi katika maeneo hayo wanaishi kwa hofu hasa wanapowaza kwamba huenda kundi hilo la kigaidi la Boko Haram likawavamia tena.

Mahitaji kama vile usalama, chakula na mavazi ni miongoni mwa yanayohitajika kwa dharura huku pia UNHCR ikibaini idadi kubwa ya wanawake wanaonyonyesha miongoni mwao wakiwamo vigori ambao wanahitaji msaada. Shirika hilo limesema miradi ya ustawi wa jamii inahitajika haraka.