Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNSOM azuru Puntland kujadili mchakato wa uchaguzi

Mkuu wa UNSOM azuru Puntland kujadili mchakato wa uchaguzi

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa mataifa nchini Somalia na mkuu wa mpango wa Umoja wa mataifa nchini humo UNSOM, Michael Keating pamoja na mwakilishi maalumu wa mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika kwa Somalia Francisco Caetano Jose Madeira wamezuru mjini Garoowe kujadili mchakato wa maandalizi ya uchaguzi na wadau mbalimbali jimboni Puntland .

Wamekutana na Rais wa Puntland Abdiweli Ali Gaas, makundi ya wanawake, viongozi wa kijadi na wagombea kiti cha Urais akiwemo Rais wa zamani wa jimbo hilo Abdirahman Faroole.

Rais wa Puntland amesisitiza kujidhatiti kwake kuhakikisha kila kitu kinakwenda sanjari na marekebisho ya mchakato wa uchaguzi, na kuongeza kuwa wamekubaliana kusalia na muda uliopangwa wa uchaguzi na kutouchelewesha zaidi.

Amesema Puntland iko tayari kutekeleza makubaliano hayo yaliyoafikiwa kwenye kongamano la kitaifa la uongozi. Bwana Keating amewataka wawakilishi wa makundi ya wanawake kuendelea na juhudi za kuchagiza asilimia 30 ya viti vya wanawake kwenye bunge lijalo la serikali ya shirikisho ya Somalia.