Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia ya kutumia mboni za macho imeanzishwa Jordan ili kuharakisha misaada: UM

Teknolojia ya kutumia mboni za macho imeanzishwa Jordan ili kuharakisha misaada: UM

Teknolojia mpya ambayo inaruhusu wakimbizi wa Syria kununua chakula kwa kutimia kumulikwa mboni ya jicho , imeanza kutumika kwenye kambi kubwa kabisa ya wakimbizi iliyoko Jordan.

Teknolojia hiyo ni mradi wa pamoja wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP na shirika la kuhudumia wakimbizi la UNHCR. Utaalamu huo ujulikanao kama iris-scan system ulifanyiwa majaribio mapema mwaka huu na sasa umeanza kutumika rasmi kwa wakimbizi 76,000 wa Syria walioko kwenye kambi ya Zaatari .

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa WFP nchini Jordan , Mageed Yahia, mradi huo umekuwa wa mafanikio makubwa na kubadili jinsi wakimbizi wanavyonunua bidhaa hasa kuwarahisishia na kwa usalama zaidi.

Utaalamu huo unatumiwa wakati wakimbizi wanataka kununua chakula kutoka kwenye maduka ya kambini kwa kutumia fedha taslimu , hundi au kadi.

Kwa upande wao wakimbizi kama Hana Heraaki, anasema imemrahisishia maisha na haimpi hofu tena kama amesahau kadi yake nyumbani, kwani akimulikwa tuu anatambuliwa.