Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban athibitisha maadili ya UM katika ahadi ya kupambana na kipindupindu Haiti:

Ban athibitisha maadili ya UM katika ahadi ya kupambana na kipindupindu Haiti:

Juhudi zaidi zinahitajika kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu nchini Haiti, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akiongeza kwamba a najutia hali hiyo akiwa kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Karibu Wahaiti 800,000 wameambukizwa kipindupindu na wengine zaidi ya 9000 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo tangu 2010 wakati kisiwa hicho kilipokumbwa na tetemeko la ardhi.

Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wameshutumiwa kuhusika na mlipuko wa ugonjwa huo na kesi kufunguliwa mwaka 2013 mjini New York ikiutaka Umoja wa Mataifa kuwalipa fidia wahanga.

Akiwa ziarani Uswisi mapema wiki hii Ban aliulizwa na waandishi wa habari jinsi gani Umoja wa Mataifa utalisaidia taifa hilo masikini, Ban akathibitisha hofu ya Umoja huo na nia yake ya kufanya kila iwezalo kuhakikisha tukio kama hilo halitatokea tena..

(SAUTI YA BAN)

"Kwa mara nyingine tena naelezea jukumu la kimaadili la Umoja wa Mataifa na kueleza majuto yangu, tulipaswa kufanya mengi zaidi ... nathibitisha ahadi ya Umoja wa Mataifa kwamba itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake, kwanza kabisa kutibu mgonjwa na kukomesha janga hili la kipindupindu, na kusaidia familia za wahanga na waathirika. "

Bwana Ban amesema mtazamo mpya kupambana na ugonjwa huo unahitajika na anatumai Baraza Kuu litaunga mkono hatua zake. Juhudi hizo ni pamoja na kutoa msaada wa vifaa kwa walioathirika na ugonjwa huo ambao unaambukizwa kupitia maji machafu na chakula, na pia kupeleka timu ya kukabiliana na mlipuko huo katika maeneo ambayo kipindupindu kimeripotiwa.

Pia kuendelea na kampeni ya chanjo, na kushughulikia suala la maji, usafi na mifumo ya afya Haiti. Takribani dola bilioni 10 zimeshachangishwa kusaidia ujenzi mpya tangu mwaka 2010, kukiwa na hali tete ya kisiasa.