Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres ang’ara kwenye kinyang’anyiro cha ukatibu mkuu UM

Guterres ang’ara kwenye kinyang’anyiro cha ukatibu mkuu UM

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limepiga kura ya sita isiyo rasmi inayotoa mwelekeo wa mgombea mmoja kati ya 13 ambaye jina lake litawasilishwa mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwania nafasi ya ukatibu mkuu wa chombo hicho.

Mara baada ya upigaji huo wa kura uliokuwa wa faragha, ukionyesha tofauti ya rangi za kura kati ya wajumbe watano wa kudumu wa baraza hilo na 15 wa kuchaguliwa, Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi wa Oktoba, Balozi Vitaly Churkin wa Urusi alizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa..

image
Balozi Vitaly I. Churkin.(Picha:UM/Loey Felipe)
(Sauti ya Balozi Churkin)

“Baada ya kura ya sita isiyo rasmi, tumepata anayekubalika zaidi na jina lake ni Antonio Guterres.”

Na kwa mantiki hiyo..

(Sauti ya Balozi Churkin)

“Tumeamua kuendelea na kura rasmi ya kupitisha jina na tunatumaini kuwa itapitishwa kwa pamoja na hilo ndilo tunatarajia, tunamtakia Bwana Guterres kila la kheri katika kutekeleza majukumu yake ya Ukatibu Mkuu kwa miaka mitano ijayo.”

Kutoka Baraza la Usalama, jina hilo litawasilishwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo wajumbe wanaweza kuidhinisha moja kwa moja au kuamua kupiga kura kwa mujibu wa kanuni za Umoja wa Mataifa.

Akizungumzia ripoti ya kuwa Guterres anan’gara zaidi kwenye kinyang’anyiro, Naibu msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema..

image
Naibu msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq.(Picha:UM/NICA ID:524389)
(Sauti ya Haq)

"Bila shaka inafurahisha kuona mchakato wa uchaguzi unaendelea kwa urahisi na kwa mpangilio"

Na kuhusu suala la kutozingatiwa mzunguko wa kijiografia na jinsia Bwana Haq amesema..

(Sauti ya Haq)

"Yeyote watakaemchagua, huyo ndiye nchi wanachama imeamua kumchagua, wao wenyewe wametoa mapendekezo yao, katika suala la uwakilishwaji wa kijiografia na suala la mwanamke kuchukua nafasi ya Katibu Mkuu, lakini ni lazima tukumbuke kwamba ni uamuzi wao, kama ilivyo kwenye katiba ya Umoja wa Mataifa, na ni lazima tuiheshimu".

Katibu Mkuu mpya anatarajiwa kuanza kazi tarehe Mosi Januari mwaka 2017 ambapo Katibu Mkuu wa sasa Ban Ki-moon anatarajiwa kuhitimisha majukumu yake tarehe 31 Disemba mwaka huu.

Naye Rais wa Baraza Kuu Peter Thomson ametoa taarifa ya kutambua kufanyikakwa kura hiyo ambayo kwa kauli moja imeonyesha Guterres kupitishwa akisema kuwa yuko tayari kusongesha mchakato huo.

Wagombea walishiriki katika mchakato wa kuhojiwa na Baraza Kuu ambapo walipata fursa ya kutoa maelezo, mchakato ulioanza mwezi Aprili.