Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalamu wa UM kuzuru Sri Lanka kutathimini hali ya walio wachache

Mtaalamu wa UM kuzuru Sri Lanka kutathimini hali ya walio wachache

Mwakilishi maalumu wa umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya walio wachache, Rita Izsák-Ndiaye, atazuru Sri Lanka kuanzia Oktoba 10 hadi 20 mwaka huu ili kutathimini hali ya sasa ya walio wachache, kitaifa, au kikabila, kidini na kilugha nchini humo.

Bi Ndiaye amesema uzoefu unaonyesha kwamba kutambua na kuchagiza haki za walio wachache ni muhimu sana katika kufikia amani ya kudumu na maridhiano hususani katika nchi kama Sri Lanka ambayo imeshawahi kugawanyika kwa migogoro ya kikabila.

Ameongeza kuwa ukizingatia chuki za muda mrefu zilizotokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 25 Sri Lanka, juhudi zozote za uwajibikaji na maridhiano ni lazima zijumuishe uangalifu wa hali ya juu ili kuhakikisha haki za makundi ya walio wachahe zinalindwa na kuchagizwa nchini humo.

Katika ziara yake ya siku 10 Bi Ndiaye atazuru Colombo na maeneo mengine ya nchi hiyo kukutana na jamii za walio wachache na kusikiliza matatizo yao. Pia atakutana na wadau wengine wakiwemo viongozi wa serikali, tume ya kitaiafa ya haki za binadamu na asasi za kiraia.

Ripoti yake ya awali na mapendekezo ataitoa kwa waandishi habari Oktoba 20, na ripoti kamili ataiwasilisha kwenye Baraza la haki za binadamu Machi 2017.