Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatuna bado ushahidi wa silaha za kemikali Jebel Marra- Ripoti

Hatuna bado ushahidi wa silaha za kemikali Jebel Marra- Ripoti

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu hali ya amani na usalama huko Darfur nchini Sudan ambapo wajumbe wamepatiwa ripoti ya Katibu Mkuu ikigusia pia madai ya hivi karibuni ya matumizi ya silaha za kemikali huko Jebel Marra.  Assumpta Massoi na ripoti kamili,.

(Taarifa ya Assumpta)

Ripoti ya Katibu Mkuu iliwasilishwa na mkuu wa operesheni za ulinzi wa usalama Herve Ladsous ambaye amezungumzia ripoti ya Amnesty International iliyosema kuwa serikali ilitumia silaha za kemikali dhidi ya raia huko Jebel Marra.

Ladsous amesema hadi sasa hawajapata ushahidi wowote wa tuhuma hizo na kwamba.

(Sauti ya Ladsous)

“Nieleze zaidi kuwa tathmini ya awali ya shirika la kimataifa la kudhibiti silaha za kemikali, OPCW imesema kuwa bila taarifa zaidi au ushahidi, haiwezekani kwa hatua hii kwa shirika hilo kuwa na hitimisho lolote kwa msingi wa yaliyomo ndani ya ripoti ya Amnesty International.”

Kwa mantiki hiyo ametoa wito kwa serikali ya Sudan ambayo ni mwanachama wa mkataba wa kudhibiti silaha za kemikali kupatia fursa shirika hilo kufanya uchunguzi kama ilivyoahidi baada ya ripoti kuchapishwa.