Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lipinge kura turufu dhidi ya uamuzi kuhusu Syria: Zeid

Baraza la Usalama lipinge kura turufu dhidi ya uamuzi kuhusu Syria: Zeid

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra'ad Al Hussein leo amesema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni lazima lichukue hatua madhubuti kuzuia wanachama wake wa kudumu kutumia kura turufu kuzuia uamuzi kuhusu hali ya Syria.

Wito huo unafuatia ongezeko la mapigano ya hivi karibuni, haswa katika mji wa Aleppo, ambapo takriban watu 270,000 wamenaswa mashariki mwa mji huo.

Hadi sasa, mgawanyiko baina ya nchi wanachama watano wa kudumu ndani ya Baraza la Usalama limezorotesha jitihada za kusitisha mapigano Syria.

Rupert Colville ni msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu, Geneva:

"Kamishna mkuu anaamini kwamba wakati wa kuonyesha uongozi wa kijasiri na vitendo imara umewadia, na kwamba baraza la usalama linapaswa, bila kuchelewa zaidi, kuweka vigezo vitakavyozuia nchi wanachama wa kudumu kutumia kura turufu, haswa pale ambapo kuna wasiwasi mkubwa kwamba uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu au mauaji ya kimbari yamefanyika. "

Pendekezo hilo litakapopitishwa, litawezesha baraza la usalama kupeleka madai ya uhalifu wa kivita katika mahakama ya kimataifa ya jinai, ICC

Halikadhalika, Kamishna Zeid amesema hatua hiyo ni muhimu zaidi wakati huu ambapo matumizi ya silaha kali katika maeneo yenye wakazi wengi mashariki mwa Aleppo na maeneo yanayoshikiliwa na serikali yamefanyika.