Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asihi Muungano wa Ulaya uridhie mkataba wa Paris

Ban asihi Muungano wa Ulaya uridhie mkataba wa Paris

Harakati za kupigia chepuo mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi zimeendelea hii leo ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelazimika kubadili safari yake ya Uswisi na kwenda Ufaransa ili kuzungumza na wabunge wa Muungano wa Ulaya.

Akiwa Strasbourg Bwana Ban amehutubia bunge hilo na kusihi lipitishe uamuzi wake wa kuchagiza kasi ya nchi za muungano huo kuridhia mkataba wa Paris na hatimaye alizungumza na wanahabari akisema..

(Sauti ya Ban)

“Hadi leo hii nchi zinazowakilisha utoaji wa asilimia 52 ya hewa chafuzi duniani zimeridhia. Na kwa uamuzi wa bunge la Ulaya hii leo, nina imani kuwa tutaweza kuvuka asilimia 55 inayotakiwa katika siku chache zijazo.

Bwana Ban amesema kwa hatua yao hii leo, wabunge wa Ulaya wamewekea msisitizo azma ya ushirikiano wa kimataifa ambao ni kitovu cha utambulisho wa Muungano wa Ulaya.