Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wapatao milioni 385 wanaishi katika umaskini uliokithiri- Ripoti

Watoto wapatao milioni 385 wanaishi katika umaskini uliokithiri- Ripoti

Watoto wako katika hatari mara mbili zaidi ya kuishi kwenye umaskini uliokithiri ikilinganishwa na watu wazima. Hii ni kwa mujibu wa utafiti mpya kutoka Benki ya Dunia na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

(Taarifa ya Rosemary)

Utafiti huo ukiangazia watoto wanaoishi kwenye umaskini uliokithiri unaonyesha kuwa mwaka 2013, asilimia 19.5 ya watoto katika nchi zinazoendelea walikuwa wakiishi katika kaya zenye kipato cha dola 1.90 kwa siku au chini, ikilinganishwa na asilimia 9.2 kwa watu wazima.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Anthony Lake anasema kuwa nusu ya watoto wote katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara na mmoja katika watoto kila watano katika nchi zinazoendelea wanaishi katika umaskini uliokithiri. Martin Evans ni mshauri mwandamizi wa masuala ya umaskini, UNICEF.

(Sauti ya Martin)

“Hii inaonyesha kuwa watoto wanajikuta kwenye hali mbaya zaidi kote ulimwenguni ambapo kile kiwango cha dola moja na senti tisini ni cha chini mno. Watoto wanajikuta bila chakula na mahitaji mengine muhimu na maisha yao, hata baada ya miaka ishirini inakuwa ni shida".

Kwa mantiki hiyo UNICEF na Benki ya Dunia wanapendekeza pamoja na mambo mengine, mara kwa mara kupima umaskini miongoni mwa watoto katika ngazi ya kitaifa na serikali za mitaa na kuzingatia watoto katika mipango ya kitaifa ya kupunguza umasikini kama sehemu ya jitihada za kukomesha umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2030.