Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marekani yatangaza kujitoa mazungumzo kuhusu Syria, UM watoa kauli

Marekani yatangaza kujitoa mazungumzo kuhusu Syria, UM watoa kauli

Mzozo wa Syria umechukua sura mpya baada ya Marekani kutangaza hii leo kuwa inajitoa kwenye mazungumzo kati yake na Urusi yenye lengo la kusaka mbinu za kusitisha chuki baina ya pande zinazokinzana huko Aleppo.

Kufuatia tangazo hilo, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura, ameelezea masikitiko yake makubwa juu ya hatua hiyo akisema ni hitimisho lisilo chanya.

Afisa kutoka ofisi ya msemaji wa Umoja wa Mataifa Eri Kaneko amemnukuu de Mistura akisema kuwa licha ya hatua hiyo, umoja huo utaendelea kusongesha suluhu la kisiasa kwenye mzozo wa Syria licha ya hatua hiyo ya kukatisha tamaa kutoka kwa wadau wawili muhimu wa kimataifa.

Halikadhalika amesema..

(Sauti ya Eri Kaneko)

“Kikosi kazi cha masuala ya kibinadau kilichoundwa na kikundi cha kimataifa cha usaidizi wa Syria, ISSG na mwenyekiti akiwa ni Umoja wa Mataifa, kitaendelea na kazi yake ili kuhakikisha hakuna vikwazo vya kufikisha misaada kwa wahitaji nchini Syria.”

Amesema Umoja wa Mataifa hautaitelekeza Syria katika mazingira ya mzozo usio na mwisho.