Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kristalina wa Bulgaria aingia kinyang’anyiro cha ukatibu mkuu UM

Kristalina wa Bulgaria aingia kinyang’anyiro cha ukatibu mkuu UM

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha kumsikiliza mgombea uteuzi wa nafasi ya Katibu Mkuu wa umoja huo Kristalina Georgieva kutoka Bulgaria ambaye aliwasilisha jina lake tarehe 29 mwezi huu.

Katika hotuba yake mbele ya wajumbe wa Baraza hilo Kuu la Umoja wa Mataifa, mgombea huyo amesema dira yake kwa Umoja wa Mataifa ni lazima uende na wakati na kuangalia upya uhalali wa uwepo wake huku ukiwapatia huduma wahitaji.

Ametaja mambo yanayopaswa kuzingatiwa kuwa ni amani na usalama, maendeleo, tabia nchi na haki za binadamu na tatu ni uongozi thabiti wa Katibu Mkuu.

Alipoulizwa kuhusu suala la amani na usalama, Bi Georgieva amesema suala hilo linabadilika na muda kwa akapendekeza mambo matatu..

(Sauti ya Kristalina)

Mosi, tuwe karibu na Afrika tusaidie Afrika kwenye uwezo wake wa kuwa na uwezo wa kupata na kupeleka vikosi haraka. Haipaswi kuchukua miezi tisa kwa kikosi cha kulinda amani kuwasilia wakati wananchi wanafariki dunia. Tuwe na uwezo wa kuchangisha fedha kwa njia endelevu na inayotabirika na pia tuungwe mkono katika uwezo wetu wa kuchukua hatua.”

Kujiunga kwa Bi. Georgieva katika kinyang’anyiro hicho kinafanya idadi ya wagombea kufikia 10 baada ya wengine watatu kujitoa.