Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kipato kwa wakulima wadogo ni muhimu- FAO

Kipato kwa wakulima wadogo ni muhimu- FAO

Kuporomoka kwa bei ya mazao kunaweza kuathiri juhudi za kimataifa za kutokomeza njaa na umasikini, endapo hatua hazitochukuliwa kuhakikisha kipato na maisha mazuri kwa wakulima wadogowadogo. Joseph Msami  na taarifa zaidi..

(Taarifa ya Msami)

Hayo yamesemwa Jumatatu na mkurugenzi mkuu wa shirika la chakula na kilimo FAO, José Graziano da Silva, ambaye ameonya kwamba, kimataifa bei ya chakula imeendelea kushuka kwa muda mrefu sasa huku ongezeko la uzalishaji likizidi mahitaji.

Da Silva amewaambia mawaziri wa kilimo na biashara  na wawakilishi wengine wa serikali wanaohudhuria mkutano wa ngazi ya juu kuhusu bei za bidhaa za kilimo kwenye makao makuu ya FAO kwamba, hali hii imechangiwa na msukosuko wa bei katika ya mwaka 2008-2012 ulioambatana na kuyumba kwa soko la chakula.

Amewaasa watunga sera kwamba wanakabiliwa na changamoto ya kuwahakikishia masikini lishe kwa gharama nafuu, huku wakihakikisha pia kipato kizuri kwa wazalishaji wakiwemo wakulima wadogowadogo.