Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utamaduni wa kupinga machafuko, unaanza kwa kuheshimu wengine:Ban

Utamaduni wa kupinga machafuko, unaanza kwa kuheshimu wengine:Ban

Kila mwaka siku ya kimataifa ya kupinga machafuko hujikita katika kuchagiza amani kwa kufuata mfano wa maisha Mahatma Gandhi ambaye alizaliwa siku hiyo, Oktoba pili , miaka 147 iliyopita. Katika ujumbe maalumu wa siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon , amesema inafahamika kwamba utamaduni wa kupinga machafuko unaanza na kuwaheshimu wengine, lakini hauishii hapo . Ili kudumisha amani ni lazima kila mtu aheshimu asili.

Ameongeza kuwa amefurahi kwamba kaulimbiu ya mwaka huu inajikita katika uendelevu na mazingira. Akimkumbuka Ghandi,  Ban amesema kwamba kila alilolifanya aliheshimu wajibu wa kila kiumbe na hivyo kumkumbusha kila mmoja wetu kua dunia inazalisha vya kutosha kwa mahitaji ya kila mtu , lakini sio kwa tamaa ya kila mtu.

Amesema Ghandhi pia alitoa changamoto kwa kila mtu kuwa chachu ya mabadiliko tunayotaka kushahududia duniani. Na kwa muktada huo amesema changamoto hiyo leo inashuhudiwa kwa vitendo, kwa India kuridhia mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabia nchi, na hakuna njia nyingine bora ya kumuenzi Mahatma Gandhi na wosia wake kwa watu na dunia kama hio.

Ban ameipongeza India kwa kuwa kinara katika mambo ya tabia nchi, na kutoa wito kwa nchi nyingine kukamilisha mchakato wa kuridhia mkataba wa Paris lakini pia kujitahidi kupiga hatua kwa njia za amani na kupinga machafuko.