Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto ya magonjwa ya moyo

Changamoto ya magonjwa ya moyo

Tarehe 29 Septemba kila mwaka dunia huadhimisha siku ya moyo. Siku ambayo wadau wa masuala ya afya wakiratibiwa na shirika la afya ulimwenguni WHO hutumia kama jukwaa la kuhamasisha kuhusu magonjwa ya moyo.

Ujumbe wa maadhimisho ya mwaka huu unalenga katika elimu kwa umma kwamba MOYO ni kitovu cha kila kitu yaani afya ambayo ndiyo uzima wa mwanadamu. WHO inataka jamii ifahamu kuwa moyo ukipata matunzo muruwa afya huwa sawia.

Katika chapisho lake shirika hilo linaelekeza ulaji unaozingatia kanuni za afya, kupunguza matumizi ya vilevi kama pombe na sigara, na ufanyaji mazoezi kama njia ya kuepukA magonjwa ya moyo.

Kwa mujibu wa WHO, zaidi ya watu milioni 17 hufariki dunia  kila mwaka  kutokana na magonjwa ya moyo, wengi wao huwa ni watumiaji wa tumbaku, kula vyakula vyenye chumvi nyingi, na kutofanya mazoezi ambapo shirika hilo limesema wengi wanaweza kuokolewa kwa kupatiwa tiba za shinikizo la damu, shinikizo la lehemu  na mengine yanayosababisha magonjwa ya moyo na kiharusi.

Hivi kariubuni WHO imetangaza mkakati wa kukabiliana na magonjwa haya shambulizi kwa moyo ambapo Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk Margaret Chan amenukuliwa akisema mkakati huo utaokoa maisha ya mamilioni ya watu kwa hatua za kuzuia magonjwa ya moyo katika jamii na katika nchi  ikiwamo kuweka ushuru katika tumbaku , kupunguza vyakula vyenye chumvi na tiba mujarabu.

Nchi zenye kipato kidogo zinatajwa kuathirika zaidi  na magonjwa ya moyo. Nchini Tanzania  hali ikoje? Tuungane na Anatory Tumaini wa redio washirika Karagwe Fm ya Kagera Tanzania.