Ban aunda bodi kuchunguza tukio la msafara kushambuliwa Syria

Ban aunda bodi kuchunguza tukio la msafara kushambuliwa Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameunda bodi itakayochunguza tukio la kushambuliwa kwa msafara wa misaada ya kibinadamu huko Urum al-Kubra nchini Syria.

Tukio hilo la tarehe 19 mwezi huu lilihusisha msafara wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na shirika la hilal nyekundu la Syria, SARC ambapo watu 18 akiwemo mkuu wa ofisi ya shirika hilo huko Urum al-Kubra waliuawa.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Ban akisema kuwa bodi hiyo ya wajumbe kutoka Umoja wa Mataifa itachunguza mazingira ya tukio hilo la mashambulizi na kumpatia ripoti.

Katika shambulio hilo, bohari ya kuhifadhi misaada iliharibiwa pamoja na kliniki iliyo karibu na eneo hilo ambapo Ban amesihi pande zote kutoa ushirikiano kwa bodi hiyo ya uchunguzi ambayo wajumbe na idadi yao haikutajwa.