Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu za usafiri ikiwemo punda zatumika kufikisha huduma Yemen

Mbinu za usafiri ikiwemo punda zatumika kufikisha huduma Yemen

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF pamoja na wadau wake wamekamilisha kampeni ya siku sita ya kufikisha huduma za afya na lishe kwa wahitaji nchini Yemen.

Kampeni hiyo ya kufika maeneo yasiyofikika, ilitumia vyombo mbali mbali vya usafiri ikiwemo magari, pikipiki, punda n ahata kutembea kwa miguu kuhakikisha kampeni hiyo ya nyumba kwa nyumba inafanikiwa.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Yemen Julien Harneis amesema kupitia kampeni hiyo watoto zaidi ya 600,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano na wanawake 180,00 walio wajawazito na wanaonyonyesha walifikiwa na huduma.

Wanawake na watoto hao walipatiwa huduma za chanjo, vidonge vya vitamin na tiba dhidi ya magonjwa ya utoto pamoja na huduma za wajawazito na waliojifungua.

Zaidi ya wahudumu 34,000 wakiwa na wasimamizi 880 walishiriki kampeni hiyo katika wilaya 333 za Yemen.