Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazingira mujarabu kwa wazee yapewe kipaumbele: UNFPA

Mazingira mujarabu kwa wazee yapewe kipaumbele: UNFPA

Mazingira bora kwa wazee na kupunguza ukosefu wa usawa kwa muda mrefu ni moja ya juhudi zinazohitajika ili kuhakikisha ustawi wa kundi hilo, dunia ikiadhimisha siku ya wazee kesho Oktoba mosi, limesema shirika la Umoaj wa Mataifa la idadi ya watu UNFPA. Rosemary Musumba na maelezo kamili.

(TAARIFA YA ROSEMARY)

UNFPA inasema katika taarifa yake kuwa watu wenye umri wa miaka 60 na kuendelea walikuwa asilimia 12.3 ya dunia mwaka jana, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 22 ifikapo mwaka 2050 na hivyo kundi hilo linapaswa kutizamwa kwani uzee hujumuisha furaha na changamoto kadhaa.

Idadi kubwa ya ongezekao la wazee inatarajiwa katika nchi zinazoendelea, huku bara Asia kwa sasa likiwa nyumbani kwa wazee zaidi ya milioni 900, miongoni mwao zaidi ya milioni 500 wakiwa na umri wa miaka 60 au zaidi.

UNFPA inasema kwa baadhi ya nchi, ongezeko la wazee laweza kusababisha kupungua kwa nguvu kazi na kusisitiza kuwa licha ya madhara yake katika uchumi, kupunguza ukosefu wa usawa na kuthamini mchango wa wazee katika maendeleo ni muhimu kwa ustawi wa jamii.