Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yasisitizia wito wa njia za kufikisha huduma Syria

WHO yasisitizia wito wa njia za kufikisha huduma Syria

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani, WHO Dkt, Margaret Chan amepazia sauti yake wito wa kuwepo kwa njia salama za kuhamisha watu wanaojeruhiwa na mashambulizi yanayoendelea nchini Syria, sambamba na kufikisha vifaa vya tiba.

Katika taarifa yake ya leo, Dkt. Chan amesema zaidi ya miaka mitano tangu kuanza kwa mapigano nchini humo vita bado inasonga akigusia zaidi mji wa Aleppo ambako vituo vya afya navyo vimezidiwa uwezo.

Akizungumzia hali hiyo mbele ya waandishi wa habari, Dkt. Rick Brennan kutoka WHO amesema.

“Tunapoangalia kile kinachoaendelea Aleppo, na tuna mawasiliano ya mara kwa mara na maafisa wa afya, hali kweli haielezeki. Kwa mujibu wa maafisa hao wiki chache zilizopita watu 338 waliuawa na mashambulizi ya mabomu, miongoni mwao ni watoto 106. Watu wengine 846 walijeruhiwa, na theluthi moja ambayo ni 261 ni watoto.”

Dkt. Brennan amesema eneo la mashariki mwa Aleppo lina hospitali sita tu ambazo hata hivyo hazitoi huduma za kutosha na idadi ya madaktari ni chini ya 30 ambayo wamechoka kimwili na kiakili.

WHO na wadau wake wanasema wana vifaa vya tiba lakini hawawezi kuvifikisha kutokana na kukosa kibali cha kuingia eneo hilo la Aleppo.