Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto Elfu 80 bonde la Ziwa Chad kufariki dunia ndani ya mwaka mmoja

Watoto Elfu 80 bonde la Ziwa Chad kufariki dunia ndani ya mwaka mmoja

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukanda wa Sahel, Toby Lanzer amesema hali ya lishe kwa watoto kwenye eneo hilo ni mbaya na ni lazima umoja huo na wadau wake zikiwemo nchi za ukanda huo zichukue hatua za haraka.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo baada ya mazungumzo yake na nchi zilizoko bonde hilo, Bwana Lanzer amesema watoto laki tano na elfu sitini na nane kwenye bonde la Ziwa Chad wana unyafuzi.

(Sauti ya Lanzer)

“Tunafahamu ndani ya miezi 12 ijayo, watoto elfu 70 au hata wapatao elfu 80 kaskazini-mashariki mwa Nigeria watafariki dunia iwapo hatutawapatia chakula chenye virutubisho cha kuwarejeshea afya.”

Bwana Lanzer amesema hakuna shaka kuwa mzozo wa Boko Haram ndio sababu kuu ya hali hiyo mbaya ya kibinadamu kwenye ukanda wa Sahel hivyo hatua za aina yake zinapaswa kuchukuliwa kuepusha janga hilo na pia lisisahaulike.