Skip to main content

UNHCR yaonya kuhusu hali ya Yei Sudan Kusini

UNHCR yaonya kuhusu hali ya Yei Sudan Kusini

Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR,limesema linazidi kutiwa wasiwasi na hali ya usalama na mustakhbali wa watu laki moja waliokwama kwenye mji wa Yei jimbo la Equatoria ya Kati Sudan Kusini. Flora Nducha na taarifa kamili.

Kwa mujibu wa duru kutoka kanisa la mji huo, watu zaidi ya 30,000, wametawanywa katika mji wa Yei na viunga vyake kufuatia mashambulizi dhidi ya raia na uporaji wa mali binafsi uliofanyika Septemba 11 na 13.

Watu hao wanaungana na wengine maelfu waliokimbia kitongoji cha Lainya katikati ya Julai, huku wengine takribani 60,000 waliosalia mjini Yei hawana njia yoyote ya kuwawezesha kuondoka na sasa wanahitaji msaada kama wakimbizi wengine wa ndani. William Spindler ni msemaji wa UNHCR

(SAUTI YA WILLIAM SPINDLER)

“Wanawake na wanaume waliojaa hofu wanasimulia  mateso dhidi ya raia kabla na wakati wa kukimbia, ikiwemo ukatili, mauaji ya kulengwa kukatwa viungo, uporaji na uteketezaji wa mali.  Raia wengi  wameuawa kikatili wakiwemo wanawake na watoto”.