Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna matumaini mkataba wa Paris kuanza kutumika karibuni- Nabarro

Kuna matumaini mkataba wa Paris kuanza kutumika karibuni- Nabarro

Matumaini ya kwamba mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi utaanza kutumika kabla ya kumalizika mwaka huu yanazidi kushika kasi baada ya idadi ya nchi zilizoridhia mkataba huo sasa kufikia 61.

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, David Nabarro amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani hii leo akisema kuwa idadi hiyo imezidi idadi inayotakiwa ya nchi 55.

Hata hivyo amesema licha ya idadi ya nchi kuzidi bado kinachotakiwa ni kiwango cha hewa chafuzi kinachotolewa na nchi hizo kiwe asilimia 55 ambapo kwa sasa jumla ni asilimia 47.79.

“Lakini unafahamu tuna imani kwa kuwa kuna ahadi kutoka angalau nchi 14 ambazo zinachangia angalau asilimia 12 ya hewa chafuzi. Nchi hizi ziliahidi kuridhia mkataba huo kupitia video iliyoonyeshwa wakati wa mjadala wa baraza kuu. Na baada ya video hizo nchi nyingine nazo zilijitokeza kuwa wataridhia. Ni kama kuna ushindani kwa nchi kujitokeza ili kuwa sehemu ya nchi zilizoridhia na kwamba ni sehemu ya mkataba ili uweze kuanza kutumika.”