Twataabishwa na ripoti kuwa Sudan imetumia silaha za kemikali- Dujarric

29 Septemba 2016

Umoja wa Mataifa umesema umetaabishwa na ripoti ya kwamba serikali ya Sudan imetumia silaha za kemikali huko Jebel Marra.

Umoja wa Mataifa umesema hayo wakati msemaji wake Stephane Dujarric alipokuwa akijibu swali la mwanahabari aliyetaka kufahamu kauli ya Umoja wa Mataifa juu ya ripoti hiyo ya Amnesty International.

Dujarric amesema wana wasiwasi mkubwa juu ya taarifa hizo kwa kuwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu, ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na muungano wa Afrika huko Darfur, UNAMID umekuwa ukiripoti ghasia huko Jebel Marra, ghasia ambazo zimeathiri raia.

 (Sauti ya Dujarric)

“Kama unavyofahamu, serikali ya Sudan imekuwa inazuia kuingia maeneo yenye mzozo huko Jebel Marra na hili limezuia ujumbe wetu kuweza kufuatilia kwa makini na kuripoti athari za mapigano.”

Hata hivyo amesema UNAMID imeimarisha uwepo wake huko Sortoni ambako raia wamekimbilia baada ya mapigano na kwamba wanatoa wito kwa serikali kuwezesha UNAMID kuingia eneo la Jebel Marra. Halikadhalika amesema..

(Sauti ya Dujarric)

“Sudan ni mwanachama wa mkataba wa kudhibiti silaha za kemikali na hivyo ukiukwaji wowote ule utachunguzwa na shirika linalohusika na silaha za kemikali, OPCW.”

Amesema kwamba OPCW ina taarifa kuhusu madai hayo ya matumizi ya silaha za nyuklia na watachunguza .

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter