Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia za Sudan zatupiwa jicho kwenye baraza la haki za binadamu

Ghasia za Sudan zatupiwa jicho kwenye baraza la haki za binadamu

Hofu kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu Sudan, leo imemulikwa katika baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi, ambapo nchi wanachama wamesikia taarifa kuhusu machafuko yanayoendelea.

Akiwasilisha ripoti yake ya karibuni kabisa, mchunguzi huru Aristide Nononsi ametanabaisha ukiukwaji mkubwa katika majimbo matatu ambayo ni Darfur, Blue Nile na Kordofan Kusini.

Bwana Nononsi ameielezea hali ya haki za binadamu katika majimbo hayo kama ni ya "hatari” mapigano yakiendelea baiana ya vikosi vya serikali na waasi waliojitenga kutoka kundi la Sudan Liberation Movement-Abdul Wahid, au SLM.

Pia ametaja kutokea kwa mauaji ya kiholela, uharibifu na uchomaji wa vijiji, kuchukua wanawake mateka na vitendo vya ukatili wa kingono kuanzia Oktoba 2015 hadi Juni 2016.

Amesema ukatili huo pia umewafungisha virago maelfu ya watu ikiwa ni pamoja na watu 80,000 kwenye jimbo la Darfur pekee walioishia kuwa wakimbizi wa ndani.

Ikijibu wito wa mchunguzi huyo kwenye baraza la haki za binadamu,wa kutaka kufanyike majadiliano huru na ya haki ya kitaifa, kwa ajili ya maridhiano nchini humo, serikali ya Sudan imesema ina nia ya kuanza tena majadiliano na makundi ya upinzani mwezi Oktoba.