Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asikitishwa na kifo cha Shimon Peres

Ban asikitishwa na kifo cha Shimon Peres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesikitishwa mno na habari za kifo cha aliyekuwa Rais wa zamani wa Israel, Shimon Peres.

Amesema, mwendazake Peres, alifanya kazi bila kuchoka katika kutafuta suluhu ya mgogoro wa muda mrefu baina ya mataifa mawili ya Israel na Palestina, kazi ambayo ilitambuliwa na ulimwengu, na hatimaye kutunukiwa tuzo ya Nobel mwaka 1994, yeye pamoja na aliyekuwa waziri mkuu wa Israel Yitzhak Rabin na rais wa zamani wa Palestina, Yasser Arafat.

Halikadhalika Ban ameongeza kuwa hata katika wakati mgumu, marehemu Peres alikuwa na matumaini ya maridhiano na amani, na akamnukuu alichokisema hapo awali,

"Wakati umefika wa kuelewa kwamba ushindi halisi utakuwa katika matunda ya amani, sio katika mbegu za vita nyingine. Tunapobadili ramani ya vita kuwa ramani ya amani, tutagundua tofauti zetu ni ndogo, na vita vilikuwa ni vya kutisha na tutagundua kwamba nchi iliyoahidiwa kumbe ingekuwa nchi ya ahadi tangu zamani sana"

Kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu Ban amesema, moyo wake shupavu uendelee kutuongoza katika harakati za kutafuta amani, usalama na heshima kwa WaIsraeli, Wapalestina na watu wote katika ukanda huo.