Skip to main content

Ban akaribisha hukumu ya ICC dhidi ya uharibifu wa maeneo ya kitamaduni Mali

Ban akaribisha hukumu ya ICC dhidi ya uharibifu wa maeneo ya kitamaduni Mali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha hukumu iliyotolewa na Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC, dhidi ya Ahmad Al Faqi Al Mahdi, aliyepatikana na hatia ya uharibifu wa makusudi wa makavazi tisa na lango la siri la msikiti wa Sidi Yahia mwaka 2012.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu inamnukuu Ban akitambua hukumu hiyo ya miaka tisa na ya kwanza kwa ICC kuhusu uharibifu wa maeneo ya urithi kwamba ni hatua muhimu katika vita dhidi ya ukwepaji sheria nchini Mali.

Ameongeza kuwa muelekeo wa kuponya majeraha kati ya jamii nchini humo lazima utekelezwe kwa uwajibikaji wa kiwango cha juu, haki na makubaliano ya amani na maridhiano.

Ban pia amelipongeza shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO , na ujumbe wa Umoja wa huo nchini Mali MINUSMA, katika kutoa usaidizi kwa mamlaka za kitaifa, katika kulinda na kujenga upya maeneo ya utamaduni wa Mali na kuhifadhi tofauti za utamaduni nchini humo.