Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azungumzia ripoti ya kutunguliwa ndege ya Malaysia

Ban azungumzia ripoti ya kutunguliwa ndege ya Malaysia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha ripoti ya awali iliyotolewa leo kuhusu kutunguliwa kwa ndege ya shirika la ndege la Malaysia, namba MH17 huko mashariki mwa Ukraine mwezi Julai mwaka 2014.

Katika ripoti hiyo ya awali jopo la pamoja la uchunguzi la kimataifa limesema ndege hiyo ilitnguliwa na kombora aina ya Buk lililorushwa kutoka Urusi.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amemnukuu Bwana Ban akirejelea azimio namba 2166 la Baraza la Usalama la umoja huo lililotaka wahusika wa kitendo hicho wawajibishwe na mataifa yashirikiane kusaka uwajibikaji.

Ameshukuru jitihada thabiti za jopo hilo lililohusisha polisi na mamlaka za mahakama kutoka Uholanzi, Ukraine, Australia, Malaysia na Ubelgiji kwa uchunguzi wa kina akisema kuwa..

(Sauti ya Dujarric)

"Tunaamini kuwa hitimisho la uchunguzi wa tukio hilo la uhalifu, pamoja na uchunguzi wa kiufundi unaoongozwa na bodi ya usalama ya Uholanzi uliobaini sababu ya kuanguka kwa ndege,vitakuwa muhimu katika kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.”